1 Peter 5

1Ninawasihi wazee waliomo miongoni mwenu, mimi, niliye mzee mwenzao na shahidi wa mateso ya Kristo, na ambaye vile vile ni mshirika katika utukufu utakaodhihirika. 2Kwa hiyo, ninawatia moyo ninyi wazee, lichungeni kundi la Mungu lililo miongoni mwenu. Liangalieni, sio kwa sababu mnapaswa, lakini kwa sababu mnatamani hivyo, kulingana na Mungu. Liaangalieni, sio kwa kupenda pesa za aibu, lakini kwa kupenda. 3Msijifanye mabwana juu ya watu waliyochini ya uangalizi wenu, lakini iweni mfano katika kundi. 4Pale Mchungaji Mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu isiyopoteza uthamani wake.

5Vilevile, nanyi vijana wadogo, nyenyekeni kwa wakubwa wenu. Ninyi nyote, uvaeni unyenyekevu na kuhudumiana ninyi kwa ninyi, kwani Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa neema wanyenyekevu. 6Kwa hiyo nyenyekeni chini ya mkono wa Mungu uliyo hodari ili kwamba awainue kwa wakati wake. 7Mwekeeni fadhaa zenu juu yake, kwa sababu anawajali.

8Iweni na busara, iweni waangalifu. Yule adui yenu, ibilisi, kama simba aungurumaye ananyatia, akisaka mtu wa kumrarua. 9Simameni kinyume chake. Kuweni na nguvu katika imani yenu. Mkijua kwamba ndugu zenu walioko ulimwenguni wanapitia mateso kama hayo.

10Baada ya kuteseka kwa muda kitambo, Mungu wa neema yote, aliyewaita katika utukufu wa milele ndani ya Kristo, atawakamilisha, atawaimarisha na kuwatia nguvu. 11Enzi iwe kwake milele na milele. Amina.

12Namthamini Silwano kama ndugu mwaminifu, na nimewaandikia ninyi kwa ufupi kupitia kwake. Ninawatia moyo na ninashuhudia kwamba nilichokiandika ni neema ya kweli ya Mungu. Simameni ndani yake. 13Waamini waliloko Babeli, waliochaguliwa pamoja nanyi, wanawasalimu, na Marko mwanangu, anawasalimu. 14Salimianeni kila mmoja kwa busu la upendo. Na amani iwe kwenu mliondani ya Kristo.

Copyright information for SwaULB